Monday, August 30, 2010

HILI LA KONDAKTA SIKULIPENDA

Jana usiku mida ya saa mbili na nusu ama saa tatu kasoro usiku nikiwa katika usafiri wetu wa kawaida daladala lifanyalo safari zake kati ya Sinza na Kariakoo nilijionea kituko ambacho kwa kweli kilinilazimisha kuchukua maamuzi magumu kuamua kwa mara moja.

Ilikuwa hivi, baada ya daladala letu kufika kituo cha Shule pale Sinza maeneo ya Mori kondakta wa daladala (minbus) tulikuwa tumepanda aliona pochi pale kituoni na kumuomba dereva wake asimamishe gari na yeye kushuka kwenda kuokota na kurudi nayo ndani ya gari (daladala). Baada ya kurudi akaanza kulipekuwa na kama kawaida watu (abiria) waliokuwemo walisema mengi kuna waliosema mwenyewe kaangusha, wengine ameshaibiwa wameamua kutupa pochi na wapo waliosema tugawane. Mie nilikuwa kimya nikitazama kinachoendele na kumsikia kondakta na abiria mmoja wa kijana wa kiume wakisema hee kuna cheti cha hospital, kuna........, kuna kadi ya benk mara kadi ya hospitali mwisho wa yote wakaamua kutupa ile pochi nje na safari kuendelea.

Hapo sasa ndipo uvumilivu uliponishinda na kuwa mkali tena sana tu kwa kumwambia dareva asimamishe gari ili kondakta afate vile vitu alivyotupa kwa kuwa ni nyaraka muhimu za muhusika na baadhi ya abiria akiwemo mzee mmoja wa makamo waliunga mkono na kondakta akaifata ile pochi, nikamwambia toa kila kilichomo tuone, kweli kuna vitu muhimu kwa muhusika. Nikauliza kama kuna anayemfahamu huyo mtu wakajibu hakuna maana kuna picha zake na kadi ya benki. Nikaamua kuamua kuchukua maamuzi magumu ya kubeba jukukumu la kumtafuta mwenyewe baada ya kuona umuhimu wa vyaraka zake.

Hilo ndo jambo lililonisikitisha baada kuona mtu anaokota kitu kwa nia flani baada ya kukuta asichotarajia anaamua kupoteza na vitu muhimu vya mwenzake. Jamani watanzania tubadilike tuheshimu nyaraka muhimu za wenzetu.

Mpaka sasa nimechukua hatua zifuatazo kumtafuta mwenye ambaye anaitwa Esther Ibrahim Shedafa, kwanza nilitangaza kumtafuta kupitia Facebook na blog ya Iaasa Michuzi. Pia blog hii nayo ilitoa tangazo hilo la kumtafuta muhusika.

2 comments:

  1. Maamuzi kama hayo yameyeyuka vichwani mwa watu, kila mtu anatamani kumpora mwenzake. Upendo, kuhurumiana na kujaliana hakupo tena, si ajabu kimuona huyo aliyepoteza akakugeuzia kibao ni kukudhani vinginevyo!
    Lakini wewe ukianza hivyo, na mwingine akafanya hivyo, baada ya siku kadhaa itajenga ule ubinadamu, kuwa cha mwenzako sio chako, ni sawa na kaa la moto, huwezi kulishika mkononi!
    Mungu akuzidishie kwa moyo huo, kwani hata mimi nilitoa tukio kama hilo jamaa kaokota pesa, alipompelekea mwenyewe akamzaba kibao na kumwambia `utakufa masikini wewe' halafu akampa kiasi kidogo kama ahsante!

    ReplyDelete
  2. Nashukuru mungu nia na madhumuni vimefanikiwa na hatimaye mwenyewe amepatika na nimemkadhi vitu vyake vyote vikiwa salama kwa mujibu maneno yake mwenyewe.

    Kweli mwanzo nilipatwa na mashaka kuwa huyu mtu anaweza kunifikilia vipi ila nikasema liwalo na liwe ila kwa bahati mwenyewe ni muelewa sana.

    ReplyDelete